Utambulisho wa Abdul-Muttalib (a.s): Alikuwa kiongozi mashuhuri wa Quraysh, mwenye hekima, heshima na hadhi kubwa katika jamii ya wakati wake. Alisimama kama nembo ya uadilifu na busara miongoni mwa Waarabu wa zama za kabla ya Uislamu.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Leo Tarehe 18 - 11- 2025, katika Msikiti wa Hawzah ya Imam Al-Hadi (as), lilifanyika Majlisi Maalum ya kuadhimisha kumbukizi ya kufariki kwa Abdul-Muttalib (a.s), babu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w). Kikao hiki kilihudhuriwa na wanafunzi, walimu na waumini mbalimbali waliokusanyika kusikiliza mawaidha na kujifunza kuhusu nafasi ya kihistoria na kiroho ya mtu huyu mkubwa katika Uislamu.

Sheikh Idris Tembo, aliyekuwa mzungumzaji rasmi wa kikao hicho cha Maombolezo, alitoa maelezo ya kina kuhusu maisha, tabia na utukufu wa Abdul-Muttalib (a.s). Miongoni mwa mambo aliyoyasisitiza ni haya yafuatayo:
-
Utambulisho wa Abdul-Muttalib (a.s):
Alikuwa kiongozi mashuhuri wa Quraysh, mwenye hekima, heshima na hadhi kubwa katika jamii ya wakati wake. Alisimama kama nembo ya uadilifu na busara miongoni mwa Waarabu wa zama za kabla ya Uislamu. -
Mlezi wa Tatu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w):
Sheikh alieleza kwamba baada ya kifo cha bibi yake na mjomba wake, Abdul-Muttalib ndiye aliyekuwa mlezi wa tatu wa Mtume. Alimlea kwa upendo mkubwa, heshima na uangalizi wa pekee, akimjua kuwa mtoto huyu ana hatima kubwa. -
Msimamizi wa Masuala ya Al-Ka‘aba:
Abdul-Muttalib alikuwa na dhamana ya kusimamia Al-Ka‘aba na shughuli muhimu za Hijja. Heshima hii ilikuwa ya juu sana, ikionyesha uaminifu na nafasi yake adhimu katika jamii. -
Mwenye Tauhid Katika Enzi za Ujahiliya:
Akiwa anaishi katika zama za ujinga na ushirikina, bado alikuwa miongoni mwa wachache waliomwamini Mungu Mmoja. Alijulikana kwa kutokutumia sanamu kama njia ya ibada, akionyesha msingi wa hali ya juu wa kiroho. -
Alikuwa Akiitwa “Ibrahim wa Pili”:
Kwa sababu ya tauhid yake, hekima na tabia zake, Waarabu walimwita “Ibrahim wa Pili,” wakimfananisha na Nabii Ibrahim (a.s) katika usafi wa imani na uongofu. -
Kufichua Mahali pa Zamzam:
Sheikh Idris Tembo alikumbusha tukio mashuhuri ambapo Abdul-Muttalib ndiye aliyegundua upya mahali pa kisima cha Zamzam baada ya kupotea kwa muda. Yeye ndiye aliyefukua ardhi na kukionyesha mahali sahihi kilipokuwa, jambo lililokuwa na umuhimu mkubwa kwa Hijja na historia ya Uislamu.
Majlis ilimalizika kwa dua maalum, katika kumuomba Mwenyezi Mungu atupe uwezo wa kujifunza kutoka katika maisha ya watu wema kama Abdul-Muttalib (a.s), na kutuongoza kuishi kwa imani, hekima na njia iliyo nyoofu.
-

Your Comment